UMUHIMU WA HADITHI KWA WATOTO
Uundaji upya wa Hadithi: Mbinu za kufundisha kusoma kwa ufahamu
Kitini cha Mwalimu cha Kujifunzia kupitia Jumuiya za Kujifunza (JzK)
________________________________________________________________________________________________________
Utangulizi
Uundaji upya wa hadithi ni mkakati wa kutumia mbinu za kufundisha ufahamu katika kuwaongoza wanafunzi kuhusianisha matukio halisi ya mazingira yao na kile kilichoelezewa katika hadithi waliyoisoma ili kuweza kupata maarifa zaidi ya kilichomo kwenye hadithi. Shughuli hii ya uundaji upya wa hadithi huwasaidia wanafunzi kutumia mbinu na mikakati ya ufahamu na kujenga stadi za lugha ili kuwasilisha ujumbe.
Mpendwa Mwalimu, jadilianeni na wenzako hoja zilizoainishwa katika kitini hiki cha kujifunzia wakati wa mkutano wa JZK.
Faida za kumsaidia mwanafunzi wa darasa la awali kuunda hadithi upya
• Hukuza ujuzi wa kuzungumza kwa watoto;
• Husaidia kuongeza uwezo wa wanafunzi kufikiri na kuhusianisha hadithi na maisha yao ya kila siku moja kwa moja;
• Hujenga kumbukumbu ya muda mrefu kuhusu hadithi aliyojifunza na mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye hadithi;
• Hukuza ujuzi wa wanafunzi wa kutumia lugha kuwasilisha ujumbe;
• Husaidia kujifunza msamiati mpya (maneno mapya); na
• Hujenga uwezo wa watoto wa kusimbua maneno katika Darasa la I.
Fuata hatua hizi ili kuwaongoza wanafunzi kuunda upya hadithi:
• Tumia kitabu au hadithi ambayo inajulikana kwa wanafunzi;
• Waambie wataje jina la hadithi au la kitabu;
• Watake wanafunzi waeleze wanachokiona kwenye jalada la kitabu;
• Uliza maswali wakati wa kuonesha picha zilizopo kwenye jalada la kitabu:
o Mnaona nini kwenye jalada?
o Picha ya jalada inatuambia nini kuhusu hadithi?
• Pitia tena maneno mapya ya msamiati:
o Waombe wanafunzi waeleze maana ya maneno mapya yaliyotumika. Kwa mfano, Roza anaposema ni hatari sana anamaanisha nini?
• Kabla ya kusoma hadithi, waoneshe wanafunzi picha za kila ukurasa. Hii inaitwa ‘mapitio ya picha.’ Uliza maswali kama:
o Ni nini kinaendelea hapa?
o Mchoro huu unakuambia nini kuhusu mhusika X?
o Unaweza kusema nini kuhusu mahali ambapo hadithi inatokea, au inafanyika?
• Baada ya mapitio ya picha, wasomee wanafunzi hadithi kila ukurasa kwa sauti. Kabla ya kuendelea na ukurasa mpya, tumia maswali ya ubashiri:
o Je, nini kitafuata?
o Unafikiri Sekelela na bibi yake wanahisi vipi kuhusu kupanda mgongo wa tembo?
o Je, Sekelela ataweza kumpanda tembo yeye peke yake?
o Uliwahi kupanda mnyama gani? Ulikuwa unaenda wapi? Ulikuwa na nani?
Utahitaji kurekebisha muundo wa maswali yako ili kuakisi hadithi husika. Maswali haya huwasaidia wanafunzi kusimulia na kuendeleza hadithi kulingana na muktadha wao halisi.
Baada ya kusoma hadithi nzima, waongoze wanafunzi kukuza stadi za kufikiri kwa kuwaongoza kujibu maswali zaidi. Waambie wajibu maswali yafuatayo wakiwa katika jozi, ili watoto wote washirikishwe na wajifunze:
o Je, ni nini kingetokea kama Sekelela na bibi yake wangeamua kutompanda tembo?
o Je, wewe umewahi kusafiri kwa kutumia usafiri wa mnyanma? Ni mnyama gani?
o Je, umewahi kuendesha nini kati ya vitu vifuatavyo? (Baiskeli, Gari, Pikipiki/Bodaboda)
o Ulikuwa unakwenda wapi?
o Ulikuwa na nani wakati unasafiri kwenda huko?
o Je, ilikuwa wakati wa likizo au la?
o Mlikuwa mnakwenda kuwatembelea akina nani? Mlipofika huko, nini kilitokea?


0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home